Jumamosi, 13 Desemba 2014

CAG akague Bodi ya Sukari- Waziri Chiza



 

Dar es Salaam, Serikali imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kukagua Bodi ya Sukari ili kubaini kama kuna aliyehusika kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje kwa mwaka 2013/14.
Kauli ya Serikali imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Kabwe kusema kuwa ataanza kulifanyia kazi sakata la sukari nchini.
Zitto alisema PAC italifanyia kazi suala hilo kwa sababu ya malalamiko ya wamiliki wa viwanda vya sukari yanayotolewa kutokana na soko la ndani kutekwa na sukari inayoingizwa kutoka nje ya nchi na wafanyabiashara wakubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alisema kuwa kazi ya kutoa kibali siyo ya waziri wala katibu mkuu bali ni ya Bodi ya Sukari hivyo kuna haja ya kufanyika ukaguzi na ikibainika kuna waliohusika wawajibishwe.
Serikali haijashindwa kupambana na wahalifu wanaoagiza sukari ya magendo, na ndiyo maana mwaka 2013/14 hakuna kibali cha kuruhusu kuagiza sukari nje ya nchi kilichotolewa cha kushangaza imejaa sokoni ina maana kuna hila imefanyika ambayo inatakiwa ibainishwe na mkaguzi mkuu.
“Atakayebainika ametoa kibali cha kuruhusu kuingiza sukari mwaka 2013/14 atawajibishwa kwa sababu taarifa zilizopo hakuna kilichotolewa na sukari imefurika sokoni, ”alisema Waziri Chiza.
Chiza alisema mahitaji ya sukari kwa mwaka ni tani 590, 000, viwanda vya ndani huzalisha tani 300,000, sukari inayoagizwa kwa ajili ya viwanda ni tani 170,000, hivyo mahitaji yanayobaki huagizwa nje ya nchi kwa vibali kutoka Bodi ya Sukari.
Chiza alisema kuwa siyo sukari tu, bali bidhaa nyingine zinaingizwa kwa magendo wengine wakitumia Bandari ya Zanzibar.
Alifafanua kuwa hiyo sukari ya magendo pia inatakiwa kuchunguzwa ubora wake kwa kuwa wengine wanatumia sukari ya viwandani kwa matumizi ya ndani , lazima wakaguzi wakague ubora na viwango vya sukari hiyo.
“Serikali haijashindwa kupambana na wanaoingiza sukari ya magendo, kama ambavyo vita dhidi ya dawa za kulevya inavyofanikiwa basi na hili linawezekana,” alisema Waziri Chiza.
Alisema mkakati mwingine ni kukata kodi sukari inayoagizwa kwa ajili ya viwanda na kuanzisha mfumo mmoja wa kutoza kodi mizigo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kuhusu malalamiko ya wamiliki wa viwanda vya sukari nchini Chiza alisema kuwa walishakubaliana kungana kuagiza sukari pamoja.

Karatasi za kupigia kura zanaswa D’Salaam


Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho nchini kote. Picha na Venance Nestory . 
Na Ibrahim Yamola na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukitarajiwa kufanyika kesho nchi nzima, wafuasi wa (Chadema) na Jeshi la Polisi, wamekamata karatasi zinazodaiwa za kupigia kura kwenye uchaguzi huo za Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, zikirudufiwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Jimbo la Ubungo, Justine Mollel, tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati mwanachama wa chama hicho alipokwenda katika duka la vifaa vya shule na ofisini saa 8 mchana kwa lengo la kurudufu karatasi za chama hicho lakini aliambiwa arudi saa 12 jioni.
Gazeti hili lilifanikiwa kuiona moja ya nakala hizo kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo ikiwa na nembo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ikiwa na nafasi ya kupigia kura kwa wagombea wa CCM na Chadema.
Habari zaidi zinaeleza kuwa tayari zaidi ya nakala milioni moja zilisharudufiwa, huku zikiwa zimewekwa alama ya ndiyo kwa mmoja wa wagombea wa vyama hivyo.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema: “Uchunguzi bado unaendelea kwani waliokuwa wanarudufu walijitambulisha kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi, hivyo tunaendelea na uchunguzi na hakuna mtu tunayemshikilia.”
Aliongeza: “Nimemwagiza OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) kuwasiliana na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili kujua hizo karatasi ni kweli zilitakiwa kutengenezwa hapo au la... Kama ni hapo mambo yaishie palepale na kama siyo halali basi hatua zichukuliwe kwa wahusika.”
Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Khalist Luanda alisema kurudufu karatasi za kupigia kura kunatakiwa kufanyika katika wilaya au mkoa lakini siyo nje ya mkoa.
“Ni kosa kuchapa fomu za wagombea kutoka wilaya moja kwenda nyingine walipaswa kurudufu katika eneo kunapofanyika uchaguzi au wilaya husika na mchakato unaopaswa kuwa wa siri sana na siyo kila sehemu kwani haitakuwa rahisi kusafirisha kwa usalama bila kutiliwa shaka.”
Aliongeza kuwa: “Nimesikia katika vyombo vya habari na nimetuma wataalamu wangu kwenda kufuatilia jambo hilo kwani ni makosa na mkurugenzi huyo inaonyesha alikuwa na malengo au masilahi binafsi na kama ni kweli anatakiwa kuwajibika.”
Awali akisimulia tukio hilo Mollel alisema: MwanaChadema alikwenda pale kurudufu karatasi zake kwani gharama yake ni Sh25 kwa karatasi moja na aliambiwa arudi jioni kwani walikuwa na kazi maalumu, hivyo wasingeweza kumrudufia karatasi zake.”
Aliongeza: “Alipokwenda tena saa 12 aliambiwa bado hawajamaliza kazi hiyo maalumu hapo alipata hofu na kuanza kuchunguza kazi iliyokuwa ikifanyika, ndipo alipoona karatasi za kupigia kura zikirudufiwa.”
Mollel alifafanua kuwa alipoona hivyo mfuasi huyo aliwaita wanachama wengine wa Chadema waliozingira duka hilo lililopo maeneo ya Mabibo kabla ya kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mabibo umbali wa takriban mita 100.

Alisema polisi wa Mabibo na baadaye wa Magomeni walipofika waliwachukua wahusika na kuwapeleka Kituo cha Polisi Magomeni kwa ajili ya kuandika maelezo.
Shuhuda ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Niliingia dukani hapo nikakuta wanachapisha hizo karatasi, lakini sikujali sana kwani nilikuwa nina haraka zangu, lakini baadaye niliporudi nikakuta baadhi ya hizo nyaraka zikiwa mezani na ndipo nikagundua kuwa ni nyaraka za siri ambazo hazitakiwi kuonekana kwa muda huo.”
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika kwa vifaa vyote kufika katika maeneo yatakayotumika kwa uchaguzi huo.
Alisema jumla ya wenyeviti wa mitaa 559 na wajumbe 2,795 wanatarajiwa kuchaguliwa. Jumla ya vituo 1,674 vya kupigia kura vitatumika huku masanduku yakiwa 5,022 na karatasi za kupigia kura zikiwa 1.7 milioni.
“Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni, tunawaomba wananchi waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura lakini wazingatie taratibu na sheria za uchaguzi,” alisema Sadiki.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, “Kila chama kihakikishe hakivunji sheria kwani hatutakuwa na hiana na mtu yeyote, ukienda kinyume tutakuchukulia hatua kali bila kujali chama ulicho na wadhifa wako.”
Aliongeza: “Tunawaomba wanawake ambao mara nyingi wamekuwa waoga kwenda kupiga kura wakihofia usalama wao kujitokeza kwa wingi kwani tumejipanga vizuri kiulinzi kuhakikisha uchaguzi unaanza na kumalizika salama.”

Al-Bashir Asema Ameishinda ICC


Rais Omar al-Bashir wa Sudan amedai ushindi katika mvutano wake na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, baada ya mkuu wa mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda, kusimamisha uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa vitani katika jimbo la Darfur.
Rais Bashir, ambaye alishtakiwa kwa mauaji ya kikabila mwaka wa 2009, alisema ICC imeshindwa katika kile alichoeleza kuwa juhudi za ICC za kuiaibisha Sudan.
Alisema wananchi wameamua kuwa afisa yoyote wa Sudan asisallim amri kwa mahakama ya kikoloni.
Fatou Bensouda alisema Ijumaa kwamba kwa vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikuchukua hatua basi wanaofanya uhalifu wa vitani Darfur wamepata nguvu kuendelea na ukatili wao hasa dhidi ya wanawake na wasichana

Mahujaji Milioni 17 Wakusanyika Karbala


Mamilioni ya mahujaji wa Kishia wamemiminika katika mji wa Karbala, Iraq, kwa ibada ya kila mwaka ya Arbaeen ingawa kuna tishio la mashambulio ya wapiganaji wa madhehebu ya Sunni wa Islamic State.
Wakuu wa Iraq wanasema mahujaji zaidi ya milioni 17 wamekusanyika Karbala kuhudhuria Arbaeen.
Picha zilizopigwa kutoka angani zinaonesha barabara zinazoelekea Karbala kama mito ya watu waliovaa nguo nyeusi, hadi upeo wa macho.
Na kuna wasiwasi kuwa mji wa Karbala hautaweza kuwapatia malazi waumini wote.
Ulinzi mkubwa umewekwa kuzuwia mashambulio ya wapiganaji wa Islamic State.
Arbaeen ni siku ya mwisho ya maombolezi baada ya kifo cha Imam Hussain cha karne ya 7 katika Vita vya Karbala - tukio muhimu ambapo Wasunni waligawanyika na Washia.

Maelfu Waandamana Washington na New York


Maelfu ya watu waandamana leo katika bara-bara za miji ya Washington na New York kupinga mauaji ya wanaume weusi wasiokuwa na silaha yaliyofanywa na polisi wa Marekani, ili kulitaka bunge lilinde wananchi.
Taarifa iliyotolewa na kiongozi wa kutetea haki za raia, Al Sharpton, ilieleza kuwa bunge linahitaji kuchukua hatua kubadilisha sheria na hali bara-barani.
Kati ya wataohudhuria maandamano hayo ni familia za Michael Brown, kijana aliyeuwawa katika jimbo la Missouri, na Eric Garner, ambaye alikufa wakati anakamatwa mjini New York.
Kesi za askari polisi waliohusika na vifo hivyo zilifutwa na kuzusha maandamano kote Marekani.

Undated photos of Michael Brown (left) and Eric Garner

.Juu ni picha za marehemu waliouawa kutoka kwa polisi nchini Marekani
A protester in Washington DC, 13 December "Mbingu inalia juu ya uvunjwaji wa haki za binadamu": Muandamanaji akiwa ameshika bango Jijini Washington DC
Protesters on a bus leaving New York for Washington DC, 13 December Mabasi yakiwa yamejaa Waandamanaji weusi kuelekea Jijini Washington na Miji mingine.
Protesters in Washington DC, 13 December "Hii tabia ikome leo": Ni msemo mwingine wa Waandamanaji.
A protester in Washington DC, 13 December  
Waandamanaji wakiendelea kupinga mauaji juu yao nchini Marekani.
Hapa inaonyesha Dunia haiwezi kukwepa desturi yake. Mara nyingi vitabu vya dini vimekuwa vikiandika kuwa binadamu wote ni sawa, lakini kwa miaka mingi sasa mwanadamu kuwa mweusi au hata kama atakuwa mweupe lakini asili yake ni Afrika amekaaliwa na mataifa ambayo watu wao wanadhani dunia hii iliumbwa kwa aajili yao.

Hafla ya kukabidhi Mgodi wa Resolute kwa Chuo cha Madini Dodoma


 Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Mhe Stephen Masele (aliyesimama katikati na pama) akishuhudia halfa fupi ya kusaini makabidhiano ya eneo la Mgodi wa Resolute kwa Chuo cha Madini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Chuo cha  Madini Dodoma, Mjiolojia Mwandamizi Subian Chiragwile, katikati ni Kaimu Kamishna wa Madini Mhandisi Ally Samaje, na kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Resolute Peter Beilby. Wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bintuni Msangi (wa pili kuchoto aliyesimama),Mkurugenzi Kampuni ya Resolute Rose Aziz na baadhi ya waliohudhuria.
 Meneja Mazingira   baada Mgodi wa Resolute Jackie Sinclair (Kulia), akimkabidhi funguo mbalimbali za majengo ya eneo la mgodi wa Resolute Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini)  Stephen Masele (Kushoto) mara  makabidhiano ya eneo la mgodi.
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Madini Dodoma Mjiolojia Mwandamizi Subian Chirangilwe funguo mbalimbali za majengo ya mgodi wa Resolute kwa ajili ya Chuo cha Madini Dodoma.
 Meneja Mkuu wa Mgodi wa Resolute Perer Beilby   (wa pili kulia) akimwogongoza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kukagua maeneo mbalimbali ya Mgodi wa Resolute ambao yamekabidhiwa kwa Chuo cha Madini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele akiangalia chumba cha Computer ambacho ni miongoni mwa vifaa ambavyo Mgodi wa Resolute umekabidhi kwa ajili ya Chuo cha Madini Dodoma.
 Meneja Mazingira wa mgodi wa Resolute Jackie Sinclair (mbelea) akieleza jambo wakati akikiabidhi baadhi ya vifaa vya maabara kwa Chuo cha Madini Dodoma. Wanaomsikiliza ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele  ujumbe alioambatana nao.
 Meneja Mazingira wa Mgodi wa Resolute Jackie Sinclair akikabidhi  moja ya vifaa ambavyo vitatumiwa na Chuo cha Madini Dodoma kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo wakati wa halfa ya kukabidhiana eneo la mgodi wa Resolute. Wanaoangalia kutoka kushoto ni Naibu Waziri  wa Nishati na Madini Stephen Masele, Kaimu Kamishna wa Madini Mhandisi Ally Samaje na Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bintuni Msangi
 Sehemu  mgodi ambao shughuli za uchimbaji zilikuwa zikifanywa na mgodi wa Resolute ambao pia umekabidhiwa kwa Chuo cha Madini Dodoma. Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo Madini Dodoma Mjiolojia Mwandamizi Subian Chirangilwe ameeleza kuwa,mgodi huo utatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu shughuli za uchumbaji.
Baadhi ya wageni waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya eneeo la Mgodi kwa Chuo cha Madini Dodoma wakifuatilia hotuba ya makabidhiano ya mgodi huo.
Chanzo:Michuzi Matukio.

RAIS MSTAAFU WA AWAMU YA PIL,ALHAJ MWINYI ATEMBELEA MIRADI MBALIMBALI YA NSSF JIJINI DAR LEO

Rais Mstaafu wa awamu ya pili nchini Tanzania,Alhaj Ali Hassan Mwinyi ametembelea miradi mbalimbali ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo aliweza kutembelea na kuangalia maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigamboni, daraja ambalo linategemea kukamilika mwezi wa saba mwaka 2015 na vilevile amepata nafasi ya kutembelea Ujenzi wa nyumba za shirika la NSSF ambao unaendelea katika eneo la Mtoni Kijichi Kigamboni na baadhi ya nyumba hizo zimeishauzwa. Pia Rais Mstaafu aliweza kutembelea ujenzi wa mji mpya wa Dege uliopo eneo la Kigamboni jijini Dar.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Injinia Abubakar Rajabu akifafanua jambo baada ya Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kufanya ziara ya kutembelea ujenzi wa Daraja la Kigamboni,Nyumba za Mtoni Kijichi na Ujenzi wa mji mpya wa Dege.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau (wa kwanza kulia) akimweleza jambo Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alipofanya ziara yake kuona ujenzi mkubwa unaodhaminiwa na NSSF
WaziriI wa Kazi na Ajira, Mh. Gaudentia Kabaka  akimkaribisha Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi  alipofanya ziara yake kwenye mirandi mbalimbali ya maendelea inayodhaminiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Meneja Mradi Mhandisi Karim Mataka akitoa ufafanuzi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi akifuatilia kwa umakini
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau akitoa ufafanuzi kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kuhusu daraja la Kiganboni
Ufafanuzi ukitolewa na Meneja Mradi wa Daraja la Kigamboni Mhandisi Karim Mattaka.
Wafanyakazi wakiendelea na ujenzi wa Daraja la Kigamboni
Meneja Mradi wa Daraja la Kigamboni Mhandisi Karim Mattaka akitoa ufafanuzi
Hii ni moja ya nguzo ambayo daraja hilo la kigamboni litakapopita
Injinia Julius Nyamhokya akitoa ufafanuzi  kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kuhusu ujenzi wa nyumba za Mtoni Kijichi/Kigamboni ambazo zimejengwa kwa hisani ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Hizi ni baadhi ya nyumba zilizoko kwenye awamu ya mwisho ya ujenzi
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau akitolea ufafanuzi wa moja ya majengo hayo 
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi akikagua ujenzi wa mji mpya wa Dege
Injinia Julius Nyamhokya akitoa ufafanuzi kuhusu vifaa vingi vinavyotumika kwenye ujenzi huo vinatengenezwa ndani ya viwanda ambavyo vimo ndani ya mradi kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau akieleza jambo kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau  akitoa ufafanuzi kwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kuhusu jengo litakalotumia kuuzia nyumba pamoja na kusimamia nyumba zote zitakazo kuwa kwenye eneo la Dege
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi akizungumza na vyombo vya habari mara baadaya kumaliza ziara yake iliyoanzia kwenye Daraja la Kigamboni, Nyumba za Mtoni Kijichi pamoja na ujenzi wa mji mpya wa Dege.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi akiagana na WaziriI wa Kazi na Ajira,Mh. Gaudentia Kabaka mara baada ya kumaliza ziara yake wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhan Dau
Huu ndio mwonekano halisi wa mji mpya wa Dege utakaokuwa Kigamboni