Dar es Salaam, Serikali imemwagiza Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali kukagua Bodi ya Sukari ili kubaini kama kuna
aliyehusika kutoa kibali cha kuagiza sukari kutoka nje kwa mwaka
2013/14.
Kauli ya Serikali imekuja siku chache baada ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Kabwe
kusema kuwa ataanza kulifanyia kazi sakata la sukari nchini.
Zitto alisema PAC italifanyia kazi suala hilo kwa
sababu ya malalamiko ya wamiliki wa viwanda vya sukari yanayotolewa
kutokana na soko la ndani kutekwa na sukari inayoingizwa kutoka nje ya
nchi na wafanyabiashara wakubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher
Chiza alisema kuwa kazi ya kutoa kibali siyo ya waziri wala katibu mkuu
bali ni ya Bodi ya Sukari hivyo kuna haja ya kufanyika ukaguzi na
ikibainika kuna waliohusika wawajibishwe.
Serikali haijashindwa kupambana na wahalifu
wanaoagiza sukari ya magendo, na ndiyo maana mwaka 2013/14 hakuna kibali
cha kuruhusu kuagiza sukari nje ya nchi kilichotolewa cha kushangaza
imejaa sokoni ina maana kuna hila imefanyika ambayo inatakiwa ibainishwe
na mkaguzi mkuu.
“Atakayebainika ametoa kibali cha kuruhusu
kuingiza sukari mwaka 2013/14 atawajibishwa kwa sababu taarifa zilizopo
hakuna kilichotolewa na sukari imefurika sokoni, ”alisema Waziri Chiza.
Chiza alisema mahitaji ya sukari kwa mwaka ni tani
590, 000, viwanda vya ndani huzalisha tani 300,000, sukari inayoagizwa
kwa ajili ya viwanda ni tani 170,000, hivyo mahitaji yanayobaki huagizwa
nje ya nchi kwa vibali kutoka Bodi ya Sukari.
Chiza alisema kuwa siyo sukari tu, bali bidhaa nyingine zinaingizwa kwa magendo wengine wakitumia Bandari ya Zanzibar.
Alifafanua kuwa hiyo sukari ya magendo pia
inatakiwa kuchunguzwa ubora wake kwa kuwa wengine wanatumia sukari ya
viwandani kwa matumizi ya ndani , lazima wakaguzi wakague ubora na
viwango vya sukari hiyo.
“Serikali haijashindwa kupambana na wanaoingiza
sukari ya magendo, kama ambavyo vita dhidi ya dawa za kulevya
inavyofanikiwa basi na hili linawezekana,” alisema Waziri Chiza.
Alisema mkakati mwingine ni kukata kodi sukari
inayoagizwa kwa ajili ya viwanda na kuanzisha mfumo mmoja wa kutoza kodi
mizigo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kuhusu malalamiko ya wamiliki wa viwanda vya sukari nchini Chiza alisema kuwa walishakubaliana kungana kuagiza sukari pamoja.
0 maoni:
Chapisha Maoni