Jumamosi, 13 Desemba 2014

Karatasi za kupigia kura zanaswa D’Salaam


Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho nchini kote. Picha na Venance Nestory . 
Na Ibrahim Yamola na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukitarajiwa kufanyika kesho nchi nzima, wafuasi wa (Chadema) na Jeshi la Polisi, wamekamata karatasi zinazodaiwa za kupigia kura kwenye uchaguzi huo za Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, zikirudufiwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Jimbo la Ubungo, Justine Mollel, tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati mwanachama wa chama hicho alipokwenda katika duka la vifaa vya shule na ofisini saa 8 mchana kwa lengo la kurudufu karatasi za chama hicho lakini aliambiwa arudi saa 12 jioni.
Gazeti hili lilifanikiwa kuiona moja ya nakala hizo kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo ikiwa na nembo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ikiwa na nafasi ya kupigia kura kwa wagombea wa CCM na Chadema.
Habari zaidi zinaeleza kuwa tayari zaidi ya nakala milioni moja zilisharudufiwa, huku zikiwa zimewekwa alama ya ndiyo kwa mmoja wa wagombea wa vyama hivyo.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema: “Uchunguzi bado unaendelea kwani waliokuwa wanarudufu walijitambulisha kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi, hivyo tunaendelea na uchunguzi na hakuna mtu tunayemshikilia.”
Aliongeza: “Nimemwagiza OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) kuwasiliana na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ili kujua hizo karatasi ni kweli zilitakiwa kutengenezwa hapo au la... Kama ni hapo mambo yaishie palepale na kama siyo halali basi hatua zichukuliwe kwa wahusika.”
Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Khalist Luanda alisema kurudufu karatasi za kupigia kura kunatakiwa kufanyika katika wilaya au mkoa lakini siyo nje ya mkoa.
“Ni kosa kuchapa fomu za wagombea kutoka wilaya moja kwenda nyingine walipaswa kurudufu katika eneo kunapofanyika uchaguzi au wilaya husika na mchakato unaopaswa kuwa wa siri sana na siyo kila sehemu kwani haitakuwa rahisi kusafirisha kwa usalama bila kutiliwa shaka.”
Aliongeza kuwa: “Nimesikia katika vyombo vya habari na nimetuma wataalamu wangu kwenda kufuatilia jambo hilo kwani ni makosa na mkurugenzi huyo inaonyesha alikuwa na malengo au masilahi binafsi na kama ni kweli anatakiwa kuwajibika.”
Awali akisimulia tukio hilo Mollel alisema: MwanaChadema alikwenda pale kurudufu karatasi zake kwani gharama yake ni Sh25 kwa karatasi moja na aliambiwa arudi jioni kwani walikuwa na kazi maalumu, hivyo wasingeweza kumrudufia karatasi zake.”
Aliongeza: “Alipokwenda tena saa 12 aliambiwa bado hawajamaliza kazi hiyo maalumu hapo alipata hofu na kuanza kuchunguza kazi iliyokuwa ikifanyika, ndipo alipoona karatasi za kupigia kura zikirudufiwa.”
Mollel alifafanua kuwa alipoona hivyo mfuasi huyo aliwaita wanachama wengine wa Chadema waliozingira duka hilo lililopo maeneo ya Mabibo kabla ya kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mabibo umbali wa takriban mita 100.

Alisema polisi wa Mabibo na baadaye wa Magomeni walipofika waliwachukua wahusika na kuwapeleka Kituo cha Polisi Magomeni kwa ajili ya kuandika maelezo.
Shuhuda ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Niliingia dukani hapo nikakuta wanachapisha hizo karatasi, lakini sikujali sana kwani nilikuwa nina haraka zangu, lakini baadaye niliporudi nikakuta baadhi ya hizo nyaraka zikiwa mezani na ndipo nikagundua kuwa ni nyaraka za siri ambazo hazitakiwi kuonekana kwa muda huo.”
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika kwa vifaa vyote kufika katika maeneo yatakayotumika kwa uchaguzi huo.
Alisema jumla ya wenyeviti wa mitaa 559 na wajumbe 2,795 wanatarajiwa kuchaguliwa. Jumla ya vituo 1,674 vya kupigia kura vitatumika huku masanduku yakiwa 5,022 na karatasi za kupigia kura zikiwa 1.7 milioni.
“Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni, tunawaomba wananchi waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura lakini wazingatie taratibu na sheria za uchaguzi,” alisema Sadiki.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, “Kila chama kihakikishe hakivunji sheria kwani hatutakuwa na hiana na mtu yeyote, ukienda kinyume tutakuchukulia hatua kali bila kujali chama ulicho na wadhifa wako.”
Aliongeza: “Tunawaomba wanawake ambao mara nyingi wamekuwa waoga kwenda kupiga kura wakihofia usalama wao kujitokeza kwa wingi kwani tumejipanga vizuri kiulinzi kuhakikisha uchaguzi unaanza na kumalizika salama.”

0 maoni:

Chapisha Maoni