WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya barabarani iliyolihusisha gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace eneo la Mlima Sekenke, wilayani Iramba kwenye Barabara Kuu ya Singida -Mwanza.
Mganga
wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Dk Antony Mbulu, alisema
kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:30 usiku wakati abiria hao wakienda
kwenye sherehe ya Maulid kijiji jirani cha Shelui.
Dk
Mbulu aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva Athuman Adam
(34) na Ally Wambura (36), wakazi wa Igunga na Amin Salim (45) mkazi wa
mjini Singida. Alisema miili ya watu wawili haijatambuliwa.
Kwa
mujibu wa Dk Mbulu, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa basi hilo
lenye namba za usajili T547 ASP kushindwa kulimudu kutokana na mwendo
kasi.
Alisema
kuwa majeruhi watano kati ya 16 waliolazwa kwenye hospitali hiyo,
wamehamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa matibabu zaidi
huku hali zao zikielezwa kuwa mbaya.
Baadhi
ya majeruhi ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walisema ajali hiyo
ilitokana na mwendo kasi na kutokuzingatia sheria za usalama barabarani.
Walidai
kuwa ajali ilitokea wakati dereva huyo akipita malori kwa kasi, ndipo
akagonga kingo za barabara na kupasua tairi kabla ya kuingia msituni na
kupinduka mara nne.
Basi hilo dogo lilikuwa limebeba abiria 21 likitoka mjini Singida kwenda Shelui.
0 maoni:
Chapisha Maoni