Dodoma. Uamuzi wa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakisusia uhitimishaji wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kimemzindua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amependekeza kubadilishwa kwa kanuni za Bunge ili kuwadhibiti.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi usiku baada ya bajeti
hiyo iliyogomewa na wapinzani kupitishwa na wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) pekee, huku akisisitiza kuwa tabia hiyo ifike wakati
ikomeshwe.
Wabunge hao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), waliamua kususia mjadala huo kwa madai ya kutoridhishwa na
ulivyokuwa ukiendeshwa kwa mikakati waliyowekeana wabunge wa CCM ya
kufukia kashfa nzito ya IPTL inayoikabili wizara hiyo.
Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe alisema
amefuatilia mjadala huo, lakini kwa bahati mbaya umegubikwa na ukinzani
wa kiitikadi na makundi, kwamba wabunge wanajadili kwa kujaribu kufukia
mambo mazito kwa sababu ya mitazamo ya makundi na kiitikadi, hivyo siyo
busara kuendelea kushiriki.
Katika maelezo yake, Pinda alisema: “Inawezekana
kanuni zinaruhusu, lakini haiwezekani kila mnaposhindwa hoja muone njia
rahisi ni kutoka nje, nasema hivi ili Watanzania waone kuwa hali hii
siyo nzuri.”
Alisema hoja zikitolewa wapinzani wanatakiwa kukaa
na kuzisikiliza na kwamba jibu siyo kutoka nje bali ni kushindana hadi
hatua ya mwisho.
“Tabia inaendelea kujengeka na siyo nzuri. Tuombe
kanuni za Bunge zirekebishwe kwa sababu Bunge linaonekana halina watu
wakati hao waliotoka hawana sababu za msingi” alisema Pinda.
Pinda aliiponda taarifa ya upinzani iliyosomwa na
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika kwamba haikuwa na jambo
la msingi na ilijaa maneno mengi.
“Mnyika ameongea maneno mengi, sikuona jambo la
msingi, angalau angechagua mambo mawili makubwa na kuyazungumza ili
tumsikie” alisema.
Akizungumzia sakata la IPTL, Pinda alisema jambo
hilo sasa linachunguzwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
(CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
kuwataka wabunge kutolijadili mpaka hapo ukweli utakapowekwa wazi.
Pinda alisema ili kuhakikisha huduma za umeme na
maji zinawafikia wananchi, amemwagiza Waziri wa Fedha kufumba macho
kutafuta fedha ikibidi hata kukata fedha za posho ili ziende katika
miradi ya maji na umeme.
“Kutokana na umuhimu wa baadhi ya sekta,
nililazimika kutoa maelekezo kwa Waziri wa Fedha. Ikiwezekana hata
tukatwe posho zote za miezi miwili maana hatuwezi kufa. Posho hizo
ziende kusaidia huko vijijini. Hili ni suala la kufa na kupona watu
hawana umeme na maji”, alisema Pinda.
0 maoni:
Chapisha Maoni