Hatimaye picha halisi ya
gharama ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) awamu ya
kwanza, imeonesha nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam kwenda na kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda
kutoka nauli ya chini ya Sh 400 ya sasa mpaka Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa
wanafunzi, nauli kwa ruti moja kwenda katika vituo hivyo vikubwa katika mradi
huo ambao utaanza kwa majaribio mwishoni mwa mwaka huu, zitapanda kutoka Sh 200
mpaka nusu ya nauli ya mtu mzima kwa ruti husika.
Aidha,
mfumo wa uendeshaji wa mradi huo na nauli, umewekwa katika sehemu mbili; sehemu
ya kwanza ni usafirishaji wa abiria kutoka maeneo ya ndani ya makazi ya watu
mpaka katika vituo vidogo na vikubwa vilivyopo barabara kuu za Dart, za
Morogoro na Kawawa kwa sasa na sehemu ya pili ni usafirishaji wa abiria kutoka
katika vituo vilivyopo katika barabara kuu ya Dart za Morogoro na Kawawa,
kwenda vituo vikuu vikiwemo Kariakoo na Posta.
Hayo
yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam, katika taarifa ya mwisho ya
Makubaliano ya Dart, iliyotolewa katika mkutano wa Mashauriano ya Uwekezaji wa
awamu ya kwanza ya mradi huo wa Dart.
Taarifa
hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika kusafiri na mabasi ya Dart kwa
safari fupi ndani ya barabara zilizo katika makazi ya watu, kwa mfano wa
barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka Shekilango, atalipa Sh 500,
tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa
atakayetumia mabasi ya Dart kutoka katika barabara ndogo zilizopo katika makazi
ya watu, kwenda katika vituo vikubwa vya Dart vilivyopo njia kuu za Morogoro na
Kawawa ili kwenda Kariakoo, Posta au Kimara, atalazimika kukata tiketi ya Sh
800, atakayoitumia kupata usafiri kutoka barabara ndogo na katika barabara
kubwa.
Mfano
wa nauli hiyo, ni abiria anayetoka maeneo hayo ya Sinza kwenda Kimara, Kariakoo
au Posta, ambaye atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, itakayomwezesha kupakia
basi la Dart kutoka maeneo hayo mpaka Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa
tiketi hiyo hiyo, kwenda Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha
kwa abiria watakaolazimika kutumia mabasi matatu ya Dart, kutoka katika
barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kupitia barabara kuu za Dart na
kwenda katika eneo lililopo katika barabara ndogo za makazi ya watu,
watalazimika kulipa Sh 900 kwa mabasi yote matatu.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, mabasi yatakayotumika kubeba abiria kwenye njia kuu,
yatachukua watu zaidi ya 150 kwa basi moja, ambapo abiria watakaopata viti vya
kuketi ni 52 na wengine wamewekewa eneo nadhifu la kusimama.
Kwa
mabasi yatakayobeba abiria kutoka njia ndogo zilizopo katika makazi ya watu,
yatachukua watu zaidi ya 80, kati ya hao abiria 42 ndio watakaopata nafasi ya
kukaa na waliobakia wamewekewa nafasi nadhifu ya kusimama.
Kuhusu
muda utakaotumika kwenye ruti moja ya mabasi hayo ya Dart, abiria atatumia muda
wa dakika zisizozidi 30 kufika anakokwenda, akitumia mabasi kwenye njia kuu,
tofauti na sasa ambapo kwa kutumia daladala abiria hutumia zaidi ya saa mbili
kufika waendako.
Akizungumza
katika mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, utaratibu wa ulipaji nauli kwenye
mabasi ya Dart, utakuwa ni wa kutumia mfumo wa kadi ambapo abiria anatakiwa
anunue tiketi kabla ya safari.
“Hakuna kulipa nauli ndani ya basi, abiria
anatakiwa alipe kabla ya kuanza safari, na kama unapanda mabasi matatu,
unatakiwa kulipa nauli yote kwa mara moja kisha unapewa tiketi, unapoingia
kwenye basi msomaji atachukua tiketi yako na kuipitisha kwenye mashine na
kupunguza nauli ya safari hiyo, hadi hatua ya mwisho wa safari,” alisema
Sagini.
Alisema
utaratibu huo, utapunguza au kuondoa kero kwa abiria na katika mabasi madogo yanayobeba abiria
kuwaunganisha kwenye njia kuu, yatakuwa
na vifaa vya mawasiliano baina ya dereva aliye barabara ndogo na dereva aliye
barabara kuu za Dart.
Kwa
mujibu wa Sagini, mradi huo ukianza, abiria watanunua tiketi kwa kupitia huduma
za fedha kwa njia ya simu kama vile M-pesa, Tigo-pesa, Pesa Fasta na Airtel
Money.
Alisema
ili kuzuia wizi na udanganyifu kwenye vituo vya mauzo ya tiketi na kwenye vituo
vya mabasi, zinafungwa kamera na video ili kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha
mapato halali kwa ruti zinazofanywa.
“Hii
itasaidia kuondoa wizi na uhujumu unaoweza kufanywa katika vituo vya abiria,”
alisema Sagini.
Alisema
kwa hatua hiyo, dalaldala za sasa zitaondolewa katika zaidi ya njia 43 ambazo
ziko kwenye barabara ya Morogoro na barabara ya Kawawa na katika ruti nyingine,
daladala hizo zitaendelea kuondolewa hadi hapo ujenzi wa barabara zote za Dart
utakapokamilika.
Katika
mabasi hayo ya kubeba abiria kwenye njia kuu za Dart, mabasi yanayoruhusiwa ni
yale yatakayokidhi vigezo, ambavyo ni pamoja na kuwa na upana wa meta 18 na
uwezo wa kubeba abiria 150, ambayo yanahitajika mabasi 145.
Kwa
mabasi yatakayosogeza abiria hadi njia kuu, yatatakiwa yawe na uwezo wa kubeba
abiria zaidi ya 80 na upana wa meta 12 na yatatakiwa mabasi 90.
Akitoa
mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema ni vyema
katika sekta binafsi, wadau wa usafiri na watu mbalimbali wachangamkie fursa
hiyo.
Alisema
Serikali kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi, umeona ni vyema
kushirikisha wadau hao kwenye mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, ambao
ukitumika vizuri ni chachu ya maendeleo na ukuaji uchumi.
0 maoni:
Chapisha Maoni