Ijumaa, 6 Juni 2014

Ugomvi wa baba na mama wasababisha kifo cha mtoto.



Polisi mkoani  Rukwa inamshikilia baba  mzazi  huku ikimsaka  mama wa mtoto mwenye umri wa mwezi mmoja, Denis Umera aliyefariki dunia kutokana na kilichodaiwa ni ugomvi wa wazazi hao uliotokana na wivu wa mapenzi.
 
Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema kifo hicho kilitokea  saa 11 alfajiri, Juni 2, mwaka huu kijijini Mlanda katika Wilaya ya Sumbawanga baada ya mama aliyekuwa amembeba mwanawe huyo, kusukumwa na mumewe na kumkandamiza mtoto.
 
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, wanandoa hao walikuwa wakipigana. Mama wa mtoto, Imelda Sindani (25) alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine.
 
Hata hivyo kulingana na maelezo ya Kamanda, wanandoa hao walikuwa na kawaida ya kugombana mara kwa mara hasa wanapotoka kilabuni kunywa pombe.
 
Kulingana na maelezo yaliyotolewa Polisi, ni kwamba mwanamke huyo alikuwa akimtuhumu mumewe kwamba tangu ajifungue, alikuwa si mwaminifu kwenye ndoa.
 
Usiku wa tukio hilo inadaiwa katika kupigana, mwanamume alimsukuma mkewe aliyekuwa amebeba mtoto. Alianguka na kumkandamiza hali iliyosababisha maumivu makali na kisha mtoto kufa papo hapo.
 
Mwaruanda alisema mwanamke huyo baada ya kugundua kuwa mtoto wake amefariki dunia, alishusha maiti na kuitelekeza na kisha kukimbilia kusikojulikana. Polisi inaendelea kumsaka.
 
Kwa upande wake, baba wa mtoto aliangua kilio kilichosababisha majirani kufika na kumkamata, kisha kumfikisha Kituo cha Polisi ambapo anashikiliwa mpaka sasa akisubiri hatua zaidi za kisheria.

0 maoni:

Chapisha Maoni