Jumanne, 22 Aprili 2014

"Hatuna mpango wa kurudi Bungeni tena....Tutakachokifanya ni kuzunguka mikoani ili `kushitaki’ kwa wananchi"..UKAWA


 
LICHA ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kuwa tayari kuzungumza na wajumbe wa Bunge hilo wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wajumbe hao wametangaza kutokuwa tayari kurudi mjini Dodoma kwa majadiliano ya aina yoyote.
 
Badala yake, umoja huo umetangaza kuendelea na dhamira ya kuzunguka katika mikoa mbalimbali nchini ili `kushitaki’ kwa wananchi, kwa kile walichodai hawajaona mwelekeo wa kutetea na kusimamia maoni ya wananchi katika Rasimu ya Katiba mpya inayojadiliwa bungeni.
 
Hayo yalisemwa jana mjini Zanzbar na viongozi wa Umoja huo, Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba kwenye Hoteli ya Mazson iliyopo Shangani.
 
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, alisema kwa sasa wanajiandaa kwenda kwa wananchi, kuelezea na kutetea msimamo wa serikali tatu.
 
“Msimamo wa UKAWA ni kwamba haturudi tena katika Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu tumeona kwamba wenzetu wa chama tawala, hawapo tayari kujadili Katiba kwa njia za kistaarabu na badala yake matusi yametawala ikiwemo ubaguzi,” alisema Mbowe.
 
Alisema wamejipanga kuzunguka nchi nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuelezea maoni ya wananchi kuhusu Katiba ambayo ni msimamo wa serikali tatu, kwa mujibu wa maoni ya Tume ya Kurekebisha Katiba, iliyokuwa chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.
 
Mbowe alisema masikitiko yao makubwa ni kwamba maoni hayo, yanapingwa katika Bunge Maalumu la Katiba na chama tawala cha CCM, chenye idadi kubwa ya wajumbe katika Bunge hilo Maalumu.
 
“Msimamo wa maoni yaliyotolewa na wananchi tangu awali ni serikali tatu kwa mujibu wa Tume ya Jaji Warioba...lakini kwa bahati mbaya maoni hayo yanapingwa na wenzetu wa CCM,” alisema Mbowe.
 
Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyegombea urais mfululizo tangu mwaka 1995, baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi, akizungumza, alisema wanatarajia kufanya mkutano mwingine mara baada ya kumalizika kwa Sikukuu ya Pasaka.
 
Alisema wamekubaliana na maombi, yaliyotolewa na Jeshi la Polisi ya kutoa nafasi kwa wananchi kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa utulivu.
 
“Hatuondoki Zanzibar hadi tufanye mkutano wetu, wenye lengo la kuwajulisha wananchi kinachofanyika Dodoma katika Bunge la Katiba ambacho ni kinyume na maoni yao,” alisema Lipumba.
 
Jeshi la Polisi Zanzibar limezuia mkutano, uliokuwa ufanywe na Umoja huo, unaoundwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na wafuasi wao walioko katika Bunge Maalumu la Katiba.
 
Hata hivyo, Jeshi hilo halikuzuia Ukawa pekee kufanya mkutano, bali hata mikutano mingine ukiwemo uliokuwa ufanywe na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), nao ulizuiwa.
 
Ukawa, baada ya kususia Bunge katikati ya wiki hii, walipanga kuzungumza nchi nzima kuelezea kile wanachodai kuonewa na `kubanwa’ katika mijadala ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, vinavyoendelea mjini Dodoma.


0 maoni:

Chapisha Maoni