Dar es Salaam. Watu watatu wamepora kiasi kikubwa cha fedha katika Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni, Dar es Salaam katika tukio linaloweza kufananishwa na sinema.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo
lililotokea jana saa tatu asubuhi, watu hao wakiwa kwenye pikipiki moja
walifika katika benki hiyo na kuiegesha nje ya uzio, kisha wawili kati
yao wakiwa na silaha waliingia ndani.
Muda mfupi baadaye, walitoka nje wakiwa na mfuko
mkubwa wenye fedha na lakini walipokuwa wakitaka kukimbia, mfuko huo
ulianguka. Hata hivyo, waliuokota na kutokomea kusikojulikana.
Mmoja wa mashuhuda, Ali Lunde alisema: “Walitoka
bila wasiwasi tena hawakupiga risasi wala kumtisha mtu yeyote. Walikuwa
na mfuko mkubwa wa ‘kisalfeti’. Walipopanda pikipiki jamaa aliyebeba
mfuko aliukumbatia kama amepakata mtoto.”
Lunde alisema wakati watu hao wakiondoka na
pikipiki, baadhi ya wafanyakazi wa benki walitoka nje huku wakipiga
kelele kuwa wamevamiwa na majambazi.
“Walitoka nje wakipiga kelele, ndipo kila mtu
akajua walikuwa ni majambazi, kama watu wangekuwa na silaha wangeweza
kuwadhibiti maana wote tuliokuwa hapa tumewaona wanavyoondoka,” alisema.
Dereva teksi anayeegesha gari lake karibu na benki
hiyo, Herode Munyi alisema aliwashuhudia majambazi hao wakiingia kwenye
benki wakiwa na silaha mkononi, jambo lililomfanya kuwapa taarifa watu
wengine huku akitafuta namba za polisi.
“Baadaye nilifanikiwa kuwaona polisi hawa
wanaotembea na pikipiki nikawaambia lakini kama vile walipitiliza,
hawakwenda moja kwa moja benki,” alisema Munyi.
Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo walionekana
kushangazwa na mazingira ya wizi huo, kwani walisema mlinzi wa benki
hiyo hakuwa na bunduki wala kirungu chochote wakati majambazi
walipovamia.
Mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka kutaja jina
lake, alisema wakati majambazi wanavamia benki hiyo, hakukuwa na watu
wengi waliokuwamo ndani, jambo lililowapa urahisi wa kutekeleza dhamira
yao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camillus Wambura alisema tawi hilo la benki halina polisi
wanaolinda baada ya benki hiyo kuwaondoa hofu kwa madai kuwa halina
biashara kubwa.
“Mwaka 2012/2013 waliondoa polisi katika benki
ambazo hazina biashara kubwa ikiwamo hii, lakini kuna haja ya kurudisha
ulinzi wa askari polisi,” alisema Wambura.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Barclays, Neema Singo alikana
madai hayo akisema benki yake ina mkataba na jeshi hilo pamoja na ile ya
Ultimate Security na kusema wameshangaa kwamba polisi hawakuwapo wakati
tukio hilo lilipotokea.
“Tuna mkataba na polisi wa kulinda matawi yote.
Tunachunguza nini kimetokea,” alisema Singo na kuongeza kwamba kutokana
na tukio hilo, tawi hili litafungwa wakati uchunguzi wa polisi
ukiendelea.
Kamanda Wambura alisema kiwango cha fedha
kilichoibwa bado hakijafahamika na kwamba hesabu zilikuwa zikiendelea
kufanywa, huku juhudi za kuwatafuta wezi hao zikiendea.
“Hakuna aliyejeruhiwa ingawa mfanyakazi mmoja amepelekwa hospitali kutokana na mshtuko,” alisema Wambura.
Mwandishi aliwashuhudia baadhi ya wafanyakazi wa
benki hiyo wakiwa wamelala kwenye gari la wagonjwa wakipatiwa msaada
baada ya kupata mshtuko. Pia polisi walionekana wakizunguka eneo hilo
huku wakiwahoji baadhi ya wafanyakazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni