Jumatano, 16 Aprili 2014

‘Lukuvi anajenga hofu kwa wananchi’



“Rais Kikwete naye alikuwa mwanajeshi, sasa kuna ubaya gani kama mwanajeshi akitawala nchi. Kuna ubaya gani mwanajeshi mwenye akili akitawala nchi yetu. Mbona Komba (Kapteni John Komba), aliwahi kuwa mwanajeshi na sasa ni Mbunge wa Mbinga Magharibi. Jeshi ni la wananchi na hao wanajeshi wanaowasema wengine huwa tunakutana nao klabu za muziki.” Joseph Mbilinyi 

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kudai kuwa iwapo mfumo wa serikali tatu utapita, jeshi litachukua nchi, wanazuoni wametafsiri kauli hiyo kuwa ni ya kuwajengea hofu wananchi.
Jumapili Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alikokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, alisema muundo huo utasababisha nchi kutawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano haitakuwa na fedha za kulipa mishahara wanajeshi.
Lakini mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mohammed Bakari amesema kauli hiyo ilitolewa katika jukwaa lisilo sahihi hususan kwa kiongozi kama Lukuvi.
“Kila kauli ina mahala pake. Haikutakiwa kwa mtu mwenye madaraka kama yule kuzungumzia mambo nyeti kama hayo kanisani,” alisema Dk Bakari.
“Licha ya kwamba kauli yake si mpya ilishasemwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, lakini ilibidi ayaseme hayo ndani ya vikao vyao na si kanisani.”
Alisema pamoja na kwamba kiongozi huyo alitoa maoni yake binafsi, ilitakiwa aangalie kwanza kauli yake kabla ya kuitoa. “Unapokuwa na nafasi ya juu ya uongozi, uhuru wako wa kutoa maoni binafsi unapungua. Kwa hiyo kupitia nafasi hiyo itabidi uzingatie masuala ya kuzungumza ukiwa raia, pia kiongozi,” alisema.
Mwanasheria Harold Sungusia alisema watu wanaodai serikali mbili wamepungukiwa na hoja na ndiyo maana wanaanzisha masuala mengine yasiyo na tija. “Nimepitia sheria zote nikagundua kuwa mtu anayetetea hoja ya serikali mbili anakosa hoja za msingi ukizingatia tayari muundo huo wa Muungano umedumu kwa miaka 50.”
Hata hivyo, mhadhiri wa Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema Watanzania hawatakiwi kuacha kufuata hoja za msingi na kutishika na propaganda. “Hizo ni propaganda kwa sababu hakuna utafiti uliofanywa na kugundua kuwa serikali tatu zitaleta vurugu.”
Mkazi wa Mbagala Mtongani, Isaiah Solomon alisema alichosema Lukuvi kinaweza kuwatisha raia hususan wale walio na uelewa mdogo juu ya masuala ya siasa.
“Si jambo jema kusemea mambo hayo kanisani. Pia alizungumzia kuhusu kugharimia jeshi, sifikiri kama ni wanajeshi pekee wanaoweza kuleta madhara iwapo fedha za kuwalipa zikiwa pungufu; wapo wafanyakazi wengine watakaoleta balaa,” alisema Solomon.
Mwenyekiti wa chama cha UDP Mkoa wa Dar es Salaam, Joackim Mwakitinga alisema woga wa wanasiasa wanaotaka serikali mbili ndiyo unaofanya watoe kauli za kuogofya wananchi.
“Naona ni woga tu wa wanasiasa wanaotaka kuleta mambo ambayo hayapo katika hoja za muundo wa Muungano,” alisema.
jumbe wa Bunge la Katiba, Joseph Mbilinyi alisema kauli hiyo inadhihirisha jinsi wanaopigia debe serikali mbili walivyo waongo.
Akichangia mjadala bungeni jana, Mbilinyi alisema: “Rais Kikwete naye alikuwa mwanajeshi, sasa kuna ubaya gani kama mwanajeshi akitawala nchi. Kuna ubaya gani mwanajeshi mwenye akili akitawala nchi yetu. Mbona Komba (Kapteni John Komba), aliwahi kuwa mwanajeshi na sasa ni mbunge wa Mbinga Magharibi. Jeshi ni la wananchi na hao wanajeshi wanaowasema wengine huwa tunakutana nao klabu za muziki.”

0 maoni:

Chapisha Maoni