Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Posted Jumatano,Aprili16 2014 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Aprili16 2014 saa 24:0 AM
Dar es Salaam. Tanzania
imeshauriwa kutotishwa na migogoro mbalimbali barani Afrika inayotokana
na rasilimali za gesi na mafuta, badala yake ifuate mipango yake
iliyojiwekea ili kuwanufaisha wananchi wote.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati na
Mabadiliko ya Tabianchi wa Uingereza, Greg Barker katika mahojiano
maalumu na mwandishi wetu nyumbani kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Barker alisema Tanzania ina bahati kupata
rasilimali hizo na kwamba zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi kwa
kuwaletea maendeleo makubwa iwapo tu hawataangalia historia ya migogoro
iliyotokana na upatikanaji wa gesi na mafuta kwenye nchi nyingine za
Afrika.
Alisema ujio wa gesi nchini utalisaidia taifa
kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira kwa kuacha kukata miti
kwa ajili ya mkaa na kuanza kutumia nishati hiyo.
Pia katika ziara hiyo iliyomkutanisha na Rais
Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge, Barker alitembelea
mradi mkubwa wa umeme wa nishati ya upepo huko Singida utakaozalisha
megawati 100 unaosimamiwa kwa ubia na Kampuni ya Aldwych ya Uingereza.
Waziri huyo aliimwagia sifa Tanzania kuwa imepiga
hatua kuwa kupambana na ukosefu wa nishati kwa kuongeza uzalishaji
kutoka asilimia 4.9 mpaka asilimia 14 kwa miaka mitatu... “Uingereza
itafanya yote yanayowezekana kusaidia jitihada hizi.”
“Kwa kusaidia sekta ya nishati rafiki kwa
mazingira Tanzania, Uingereza itafanya kazi kwa karibu… Hii ni muhimu
kuhakikisha joto la wastani halitaongezeka juu ya nyuzi mbili zaidi ya
viwango vya kabla ya viwanda,” alisema.
Balozi wa Uingereza nchini, Diana Melrose alisema
Tanzania ina fursa kubwa ya kuimarika kiuchumi kutokana na rasilimali
mbalimbali ilizonazo kwa kuwa inaungwa mkono wa mataifa makubwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni