Alhamisi, 10 Aprili 2014

VIPORO VILIVYOBAKI VIFANYIWE KAZI -TANZANIA



Na  Mwandishi Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imesisitiza kuwa,  Mpango wa Utekelezaji kuhusu Idadi ya watu na Maendeleo (ICPD)  unapashwa  kuzingatia pamoja na mambo mengine  umalizaji  wa   ajenda  ambazo hazijakamilika au kwa maneno mengine viporo vilivyobaki.
Tanzania  imevitaja viporo hiyo kuwa ni  upunguzaji wa umaskini,  tofauti za usawa wa jinsia,  elimu kwa watoto wa kike,  uimarishaji wa huduma za afya,  utokomezaji wa  magonjwa mbalimbali  yakiwamo  malaria,  kifua kikuu na maambukizi ya virusi ya Ukimwi.
Msisitizo huo wa Tanzania umetolewa na  Bw. Charles Pallangyo, Katibu Mkuu, Wizara ya  Afya na Ustawi wa Jamii, katika siku ya tatu ya Mkutano wa   47 wa Tume ya Idadi ya Watu na Maendeleo, (ICPD)  unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
 Katibu Mkuu  Pallangyo  anaongoza  ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika  Mkutano huo  ambapo washiriki  wanaoziwakilisha   Serikali zao , wanafanya  tathmini  ya  hali ya utekelezaji wa Mpango wa  Utekelezaji wa Mkutano  wa Kimataifa kuhusu  Idadi ya Watu na  Maendeleo uliofanyika miaka 20 iliyopita huko  Cairo,  Misri.
“ Tanzania  imejitahidi  sana na imefanikiwa  katika utekelezaji wa  Mpango wa Cairo,  yapo maeneo ambayo tunajivunia ,nayo ni,  upunguzaji wa  idadi ya vifo vya watoto wachanga,  kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika ngazi za utoaji wa maamuzi  kama vile  Bunge na taasisi nyingine,  fursa sawa za elimu kwa uwiano wa jinsia,  uwezeshwaji wa wanawake na  haki za binadamu kwa uchache” akasema katibu Mkuu na kuongeza.
Pamoja na  mafanikio hayo na mengine mengi,  bado kuna maeneo ambayo   mafanikio yake  si ya kuridhisha sana. Baadhi ya  maeneo hayo ni  upunguzaji wa vifo vya wanawake wajawazito na  utokomezaji wa magonjwa kama vile  maambukizi ya  virusi vinavyosababisha  ukimwi.
“  Ni kwa sababu hiyo basi,  sisi ( Tanzania) tunataka kutilia mkazo  kwamba,  kima ilivyokuwa miaka 20 iliyopita,  ICPD ni muhimu sana hasa  katika  maandalizi ya ajenda za maendeleo endelevu  baada ya 2015.  ni lazima pia kutilia mkazo utekelezaji wa  viporo ambayo havikumalizwa wakati wa utekelezaji Malengo ya Maendeleo ya Millennia ambayo yanafikia ukingoni” akasisitiza Katibu Mkuu Pallangyo.
Akaogeza kwamba,  Mpango wa Utekelezaji wa ICPD ni vema pia ukashughulikia changamoto mpya zinazoibuka hivi sasa zikiwamo za uongezeko la  idadi ya wazee ,ongezeko ambalo linapita idadi ya watoto wadogo chini ya miaka mitano.
Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania,  ni  kati ya nchi  47  zilizochaguliwa na  Baraza Kuu la Uchumi na Ustawi wa Jamii ( ECOSOC) kuwa  mjumbe wa Tume  ya Idadi ya Watu na Maendeleo.  Wajumbe  hudumu wa katika Tume hiyo kwa  kupindi cha miaka mine na  huchaguliwa kwa mgawanyo wa  kijiografia.
 Pamoja na wajumbe wanaotoka  serikali mbalimbali, mkutano huu  unahudhuriwa pia na  idadi kubwa  ya wajumbe  kutoka  Asasi zisizokuwa za kiserikali.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizowasilishwa  wakati  wa mkutano huu zinazonyesha kwamba  kwa  ujumla kumekuwapo na mafanikio makubwa  katika kipindi hicho cha miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano huo wa Cairo mwaka 1994.
Baadhi ya mafanikio hiyo ni  kuongezea kwa umri wa watu kuishi ambapo sasa dunia inasadikiwa kuwa na wazee wengi, kuongezea kwa wakazi wa mijini, kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, wanawake kujipatia fursa ya kimiliki ardhi katika baadhi ya nchi,
 Katika  Mkutano huo wa  Kimataifa wa Cairo ambao unatajwa  kuwa ni  mkutano wa kihistoria,  uliohudhuriwa na  nchi 179 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo  mkazo   ulikuwa kwamba  binadamu ndiye mlengwa mkuu  katika jitihada za  kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii
 Ni katika Mkutano huo ambapo suala la  upatikaji wa huduma za elimu , afya na haki za binadamu hasa wanawake na vijana kulielezwa  kama kungesaidia uchagizaji wa  maisha bora kiuchumi na kijamii na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo endelevu na  mwenendo endelevu  wa idadi ya watu
Aidha  wakati wa mkutano huo wajumbe walijiwekea malengo ya utekelezaji katika maeneo ya  upunguzaji wa umaskini,  utokomezaji wa tofauti za kijinsia,  maendeleo ya miji na  uhamiaji,   maendeleo ya jamii,  na haki za wanawake  na vijana katika  maeneo mbalimbali kama vile haki za  afya pamoja na afya ya uzazi.

0 maoni:

Chapisha Maoni