Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kuomboleza kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa, Ndugu Moshi Chang’a.
“Ni
kifo cha kusikitisha kwa sababu kimepunguza safu ya uongozi wetu na
kimelinyang’anya taifa letu mhamasishaji hodari na mtetezi wa kuaminika wa
maendeleo ya wananchi,” Rais Kikwete amesema katika
salamu hizo.
Amesema
Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi: “Nilimjua Ndugu Chang’a kwa miaka
mingi tokea mwaka 1979 alipojiunga na utumishi wa Chama cha Mapinduzi ambacho pia
alikitumia kwa uaminifu mkubwa hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka
2003. Alikuwa kiongozi wa kweli kweli wa maendeleo na kifo chake kimetuachia
pengo la uongozi.”
“Nakutumia
salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako, naitumia
familia wa Ndugu Chang’a pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na
mhimili wa familia. Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika
kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu kwa sababu yote ni mapenzi ya
Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema,
aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais
katika salamu hizo.
Ndugu
Moshi Chang’a ambaye aliaga dunia jioni ya jana, Jumapili, Aprili 20, 2014 katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar Es
Salaam amekuwa mkuu wa wilaya katika Mikoa ya Mbeya, Tabora na Rukwa.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
21
Aprili,2014
0 maoni:
Chapisha Maoni