Alhamisi, 17 Aprili 2014

MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WAKAZI WA KATA YA MSINJAHILI KUTOOGOPA KUVUTA UMEME MAJUMBANI MWAO

Thursday, April 17, 2014


Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Wakazi wa kata ya Msinjahili wilayani Lindi wametakiwa kutoogopa kuvuta umeme majumbani mwao kwa kuhofu kuwa wakifanya hivyo wataonekana ni matajiri kwani matumizi ya umeme ni ya gharama naafuu ukilinganisha na  mafuta ya taa.

Mwito huo umetolea jana na  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini wakati akiongea  kwa nyakati tofauti  na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya  Muungano, Jitegemee, Sinde na Mnali yaliyopo katika kata ya Msinjahili wilaya ya Lindi mjini.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema ili kuboresha  maisha ya wananchi Serikali imejitahidi kupitisha  umeme wa gesi katika  vijiji vilivyopo katika kata hiyo na kupunguza gharama ya uvutaji ambazo ni nafuu  jambo la muhimu ni kwa wananchi kuutumia.

“Kuwa na umeme nyumbani kwako na kuutumia ni mwanzo wa maendeleo,  hata watoto wako wataweza kuutumia mwanga huo kwa kujisomea hasa nyakati za usiku  na hivyo kufanya vizuri katika mitihani yao”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mjumbe huyo wa NEC  pia aliwataka  viongozi hao  wa Halmashauri kuu ya tawi kuwahimiza watu wanaowaongoza katika maeneo yao kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kulima chakula cha kutosha jambo ambalo litawafanya kuwa na chakula cha ziada na hivyo kuepukana na kitendo cha  kuomba chakula kwa majirani.

Akizungumzia kuhusu suala la uongozi Mama Kikwete aliwahimiza  wanawake kutoogopa kuomba na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi  katika chaguzi zijazo ili waweze  kupata nafasi ya kuongoza na hivyo kufika katika ngazi ya maamuzi.

Mama Kikwete alisisitiza , “Sisi wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi  na mtu pekee anayeweza kuziongelea changamoto zetu kiusahihi ni mwanamke mwenyewe hivyo basi msiogope kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi ukifika mkifanya hivyo kutakuwa na viongozi wengi wanawake ambao wataweza kuwakilisha matatizo na mawazo yetu katika ngazi za juu za uongozi wa chama na Serikali”.

MNEC huyo alimalizia kwa kuwahimiza viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kuishi maisha ya  upendo, mshikamano na amani kwani jamii ikiishi maisha hayo itaweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana.

Kwa upande wake  katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Lindi Haji Tajiri aliwataka viongozi hao kuwa  waaminifu katika ndoa zao  na kuepuka tabia ya kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja (michepuko) kwa kufanya hivyo  wataepukana na ugonjwa wa Ukimwi.

“Chama Cha Mapinduzi  kinahitaji kuwa na watu wenye afya njema ili waweze kufanya vizuri kazi za chama nawaomba muwe waaminifu kwa wapenzi wenu mkifanya hivyo mtaepekana na Ugonjwa wa Ukimwi”, alisema Tajiri.

Katibu huyo wa Jumuia ya Wazazi mkoa pia aliwaomba  kinamama  kuiga  mfano wa Mama Salma Kikwete ambaye anafanya kazi kubwa ya kujitoa katika shughuli mbalimbali za kijamii na kutetea haki zao, wasichana  na watoto na kuongeza  kwamba   anastahili pongezi kwani  yeye ni mama na mlezi wa taifa.

Mjumbe huyo wa NEC taifa akiwa katika kata ya Msinjahili alifungua mashina ya wakereketwa wa CCM Jumuia ya wazazi  katika tawi namba  tatu  la Sinde na namba mbili  la Mnali.

Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi.

0 maoni:

Chapisha Maoni