Jumanne, 15 Aprili 2014

WANANCHI KUNUNUA MAFUTA YA GARI KUPITIA M PESA


Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma ya kulipia mafuta kwa Mpesa kwenye vituo vya mafuta vya Total nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara wa Total Romee de Villeneuve. Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dra es salaam.  
Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania,Salum Mwalim akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi ya kulipia mafuta kwa Mpesa kwenye vituo vya mafuta vya Total muda mfupi baada ya kuzinduliwa rasmi kwa huduma hiyo kwenye kituo cha Total cha Morocco jijini Dra es salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara wa Total Romee de Villeneuve. Huduma hiyo itakuwa ikipatikana kwenye vituo vyote vya Total hapa nchini.
Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim (wa pili kushoto) akimsadia dereva Taxi Said Juma kulipia mafuta kwa njia ya M-pesa katika kituo cha Mafuta cha Totola Morocco jijini Dar es salaam akiwa ndie mteja wa kwanza kutumia huduma hiyo muda mfupi baada ya kuzinduliwa kituoni hapo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Biashara wa Total Romee de Villeneuve na kulia ni mhudumu wa kituo hicho Malaki Peter. Huduma hiyo itakuwa ikipatikana kwenye vituo vyote vya Total nchini.
Wafanyakazi wa Vodacom wa idara ya mauzo wakibandika stika kwenye kituo cha mafuta cha Total Morocco jijini Dar es salaam zinazoonesha nambari ya biashara ya kulipia huduma ya mafuta kwa njia ya Mpesa kituoni hapo. Huduma hiyo imezinduliwa kituoni hapo na kwamba itapatikana kwenye vituo vyote vya Total nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa Vodacom kuwawezesaha watanzania kupata huduma kwa urahisi, uhakika na usalama kupitia huduma ya M-pesa.
Mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha Total Morocco jijini Dar es salaam akitoa huduma ya mafuta kwa wateja. Total na Vodacom imezindua ubia wa kibiashara unaowawezesha wateja kulipia huduma ya mafuta kwa M-pesa kwenye vituo vyote vya Total nchi nzima. Huduma hiyo inalenga kutoa unafuu na urahisi wa malipo kwa wateja.

Waendesha vyombo vya moto barabarani wamerahisishiwa njia ya kununua na kulipia mafuta kwa njia ya M-Pesa, kufuatia ushirikiano kati ya kampuni ya simu za mkononi Vodacom M-Pesa na kampuni ya uuzaji na usambazaji wa mafuta ya Total Tanzania.

Ushirikiano huo umeanzia kwenye vituo vichache vya Total Tanzania na baadae kusambaa maeneo mbalimbali nchini, lengo kuu ni kuhakikisha kila mtanzania anaemiliki chombo cha moto anakuwa na uwezo wa kununua na kulipia mafuta kwa njia iliyo salama na uhakika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim, amesema siku zote kampuni yake imekuwa msitari wa mbele katika kurahisisha maisha ya Watanzania kupitia miundombinu ya kiteknolojia iliyo nayo.

"Tumekuwa tukibuni njia mbalimbali kila siku kwa lengo la kuwapa urahisi wateja wetu na kuwaondolea adha ambazo wanaweza kuzipata wakiwa wanataka kununua mafuta kutoka vituo vya Total Tanzania, sasa wateja wetu wote kupita M-Pesa ambayo siku izi imechukua nafasi kubwa sana katika mfumo wa maisha ya binadamu wana uwezo wa kununua na kulipia mafuta kutoka vituo ivyo vya mafuta." Alisema Mwalim

Aidha, Mwalim aliongeza kuwa kampuni ya Vodacom kupitia M-Pesa wataendelea kuwaletea wateja mambo mengi ambayo hayajawahi kutokea nchini, lengo likiwa ni kuhakikisha biashara zote nchini zimeunganishwa na M-Pesa ili kwenda sambamba ambapo hadi sasa tayari biashara zaidi ya 320 zimeshaunganishwa na huduma hiyo.

"Tunatambua watu wengi wanahitaji la kununua mafuta kwa ajili ya magari au piki piki zao lakini kwa bahati mbaya wanaweza kufika kwenye kituo cha mafuta wakiwa na fedha pungufu, sasa wasiwe na wasi wasi wowote endapo watakuwa na fedha katika akaunti zao za M-Pesa wanaweza kutatua tatizo hilo". Alisisitiza Mwalim.

Kwa upande wake Meneja wa Maendeleo, Ubora na Mafunzo wa Kituo cha mafuta cha Total Tanzania, Maria Lebby, Amesema kupitia njia hii wateja wa Total watanufaika kutokana na namna kampuni hiyo ilivyo jidhatiti katika kurahisisha njia za malipo.

"Tumekuwa tukipokea wateja mbalimbali kwa nyakati tofauti zikiwemo za usiku ambazo ni hatarishi kwa usalama wa fedha alizobeba mteja, hivyo basi kuanzia sasa mteja wetu anaweza kutembea bila yakubeba fedha taslimu na badala yake kuziweka kwenye akaunti yake ya M-Pesa na kujihakikishia anapata huduma akiwa na amani juu ya usalama wa fedha zake."

Aidha Meneja huyo aliendelea kubainisha manufaa watakayopata wateja kwa kusema "huu ni wakati wakutumia teknolojia tulizonazo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watanzania, waliowengi wanapenda kufanya mambo yao kwa uharaka hasa wanapokuwa na majukumu mengine yakufanya, kupitia huduma hii tatizo hilo litakuwa limetatuliwa".

"Natoa wito kwa makampuni mengine kukubali kupokea mapinduzi yanayoletwa na teknolojia ili kuweza kwenda na wakati na kurahisisha mfumo mzima wa upatikanaji wa huduma". Alihitimisha Lebby.

0 maoni:

Chapisha Maoni